STORY:WAMEGOMBANA, WANATAKA KUACHANA? WE’ INAKUHUSU NINI?



Ni Ijumaa nyingine nzuri tunapokutana tena nawe msomaji wangu, nategemea uko poa kwa kudra za Mungu na unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku. Karibu kwenye uwanja wetu huu na leo nataka kuzungumza nawe mada ya tofauti kidogo.

Jambo lenyewe ninalotaka kuzungumza nawe msomaji wangu, ni tabia waliyonayo baadhi ya watu ya kushadadia matatizo ya kimapenzi yanayotokea kwenye maisha ya watu wao wa karibu, wawe ndugu, marafiki, majirani au watu ambao wanachangamana nao kwa namna moja au nyingine.
Yaani mtu wako wa karibu amekorofishana na mwenzi wake, wewe badala ya kutoa ushauri mzuri au kunyamaza kimya kama huna ushauri wa kujenga, matokeo yake unashadadia na kuendelea kumwaga sumu ili ugomvi uzidi kuwa mkubwa au waachane kabisa.

Bila shaka msomaji wangu utakuwa umeshakutana na watu wa aina hii ambao wao kazi yao kubwa ni kushangilia matatizo ya wenzao au yawezekana wewe pia ni miongoni mwa watu wa aina hiyo.
Siri kubwa ambayo huijui, wahenga wanasema ndugu wakigombana chukua jembe ukalime. Watu wanaopendana kwa dhati, ambao wameshaishi pamoja au wana ndoto za kuja kuishi pamoja, wanakuwa sawa na ndugu.

Inapotokea wakagombana, kuwa makini sana usishadadie matatizo yao. Kama una busara, simama katikati kujaribu kuwashauri wamalize tofauti zao ili maisha yaendelee.
Lakini kama kazi yako ni kuchochea kuni, kuongeza chumvi na kutoa ushuhuda wa uongo ili tu wazidi kugombana na mwisho waachane, elewa kwamba mwisho wake utaadhirika.

Mapenzi ya kweli huwa hayafi kirahisi hata kama yamekumbwa na kimbunga kikubwa kiasi gani. Hujawahi kuona mume amezaa nje, mke amejua na ugomvi mkubwa umetokea kiasi cha kufikia hatua ya kutaka kutengana lakini mwisho wanayamaliza na maisha yanaendelea, tena kwa upendo kuliko mwanzo?

Hujawahi kuona wenza wanakoseana makosa makubwa-makubwa, wanapigana na kudhalilishana kiasi kwamba kila mtu anajua wamefika mwisho lakini baada ya kila mmoja kukaa na kutulia, wanarekebisha kasoro na maisha yanaendelea, tena kwa mahaba mazito kuliko mwanzo?

Nakupa mifano hii ili uelewe kwamba nguvu ya mapenzi ya kweli ni kubwa sana. Linaweza kutokea tatizo kwa wanandoa au wenzi ambao unawajua, ukajiaminisha kwamba hawawezi kurudiana tena, ukachochea kuni na kuongeza chumvi kadiri uwezavyo lakini mwisho ukawaona wako pamoja tena, mahaba yakiwa yamekolea kuliko mwanzo.

Wakishapatana, wataambizana yale yote uliyokuwa unayasema, kila mmoja atamueleza ukweli mwenzake juu ya nani na nani walikuwa wanashadadia waachane. Hujanunua ugomvi na chuki kali mpaka hapo?
Kama wewe ni mtu unayejiheshimu, mwenye busara na usiyetaka matatizo na binadamu wenzako, unapaswa kujizuia sana kushadadia matatizo ya kimapenzi yanayowatokea watu wako wa karibu.
Hata kama mmoja kati yao amekufuata kuomba ushauri, jitahidi sana ushauri wako uwe ni wa kujenga na kumaliza tofauti kati yao. Usimshauri mtu aachane na mwenzi wake kwani mwisho wa siku, uamuzi unabaki kwake mwenyewe.

Ni makosa sana kuanza kumhadithia mabaya ya mwenzi wake mtu ambaye yupo kwenye matatizo. Kauli mbaya kama za ‘huyo ameshindikana, watu kibao wamepita hapo utakuwa wewe?’, ‘yule mwanamke malaya sana, hakufai’ au ‘huyo siyo mume, anakupotezea muda wako tu’ ni sumu kali ambayo unapaswa kuizuia isitoke kupitia kinywa chako.

Walipokutana hukuwepo, umeanza kuwaona tu wakiwa pamoja kwa hiyo maisha yao hayakuhusu. Badala ya kupoteza muda wako kukoleza makaa kwenye penzi lao linaloyumbayumba, ni vyema ukaelekeza nguvu kulinda penzi lako ili na wewe yasije kukukuta kama yanayowatokea wenzako.

Kwa leo niishie hapa, kwa ushauri, maoni nicheki kwa namba za hapo juu. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright VIJIMAMBOZI Published.. Blogger Templates
Back To Top