ZITTO KABWE AFUNGUKA KUWA ALIPOFUKUZWA CHADEMA ALITAMANI KUJIUNGA NCCR-MAGEUZI.....SOMA HAPA

 
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amefunguka na kusema kuwa alipofukuzwa Uanachama katika chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alitamani kujiunga na Chama Cha NCCR-Mageuzi kwani ndicho chama ambacho kilikuwa kinaendana na itikadi yake anayoifuata na kuiamini ambayo ni itikadi ya Ujamaa.

Zitto Kabwe alifunguka haya jana alipokuwa akichat Live kupitia ukurasa wa facebook wa EATV katika kipengele cha KIKAANGONI .



Zitto Kabwe alisema kuwa alishindwa kujiunga na Chama hicho cha NCCR-Mageuzi kutokana na kuwepo kwa matatizo hivyo aliona siyo vyema kujiunga nacho, ndiyo maana alifikiri kuwa na chama cha siasa ambacho kitakuwa na misingi na itikadi ambayo yeye anaiamini na kuisimamia. 

Katika hili moja ya shabiki alitaka kujua kwanini aliamua kujiunga na ACT Wazalendo na kuacha kujiunga na chama kilichokomaa kisiasa kama TLP,NCCR-Mageuzi,CUF, au CCM na majibu ya Zitto yalikuwa kama hivi.

"Nilifikiria hivyo pia lakini nikaona kuwa ni vema sasa kuwa na chama cha siasa ambacho kina itikadi ninayoifuata na kuiamini nayo ni itikadi ya Ujamaa.

"Chama cha NCCR-M mageuzi pekee ndio kinakaribia kuwa na itikadi hiyo lakini napo kulikuwa na matatizo ambayo kujiunga kwangu nao ingekuwa sio vema. Pili mimi ni mpiganaji. 

Wengine wananiita jeshi la mtu mmoja! Sio kweli lakini. Hivyo kwenda chama kichanga ni ujasiri wa hali ya juu. Mungu atasaidia hakitakuwa chama kichanga baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2015".

"Mimi sio mwanzilishi wa ACT Wazalendo isipokuwa waanzilishi walikuwa watu ninaoshabihiana nao kwenye itikadi kama Prof. Kitila Mkumbo na Ndugu Mwigamba" Aliongeza Zitto Kabwe.

Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo ambaye kwa sasa amekuwa akiitwa majina mengi ya ajabu ajabu kama msaliti,Yuda, kibaraka wa CCM na mengine mengi alisema kuwa hilo ni suala la kawaida katika siasa maaana hayo ni maneno tu ambayo hata baadhi ya viongozi wakubwa katika vyama vya siasa walishaitwa majina hayo ila anasisitiza jambo kubwa na la muhimu ni kumpima kwa kazi zake ambazo amezifanya bungeni katika kipindi chote alipokuwa mbunge na jinsi alivyoweza kujenga uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi.

"Hayo ni maneno ya kisiasa tu. Hata Marando aliwahi kuitwa Msaliti. CUF waliwahi kuitwa mashoga. NCCR na Mbatia waliwahi kuitwa pandikizi. 

"Ni maneno ya kisiasa tu ambayo hayaongezi ugali kwenye sinia. Muhimu ni kuni judge kwa kazi ambazo nimefanya Bungeni katika kipindi changu. Kazi ya kujenga uwajibikaji." 

Lakini mbali na kuonyesha kuwa kumekuwa na changamoto katika siasa za Tanzania hususani ndani ya vyama vya siasa Zitto Kabwe alizidi kusisitiza kuwa chama cha siasa ni itikadi hata hivyo umoja wa vyama vya siasa ni muhimu sana katika kujenga Demokrasia imara.

"Chama cha siasa ni itikadi. Hata hivyo umoja wa vyama ni muhimu sana katika kujenga demokrasia imara"

Uchaguzi Mkuu 2015
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo ameonyesha kuwa huenda kwa mwaka huu katika uchaguzi mkuu Tanzania ikaandika historia nyingine kwa Rais wa chama kimoja kukabidhi nchi kwa Rais wa chama kingine, hii inamaana kuwa huenda Rais Jakaya Kikwete akakabidhi nchi kwa Rais kutoka chama cha upinzani.

"Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Rais wa chama kimoja anaweza kukabidhi nchi kwa Rais kutoka chama kingine." 

Lakini hapo hapo kiongozi huyo ndipo alipoonyesha wazi kuwa kwa upande wake yeye atagombea nafasi ya ubunge kupitia chama chake cha ACT Wazalendo na kusema kuwa mpaka sasa hajajua ni jimbo gani anakwenda kugombea nafasi hiyo ya ubunge. 

"Nitagombea Ubunge mungu akipenda. Jimbo gani bado sijaamua" 

Kutokana na hili mashabiki walihitaji kujua siku akiweza kufanikiwa kushika nafasi ya Rais wa nchi hii ni jambo gani la kwanza kuanza kufanya .

"Ikitokea nimekuwa Rais wa Tanzania Kila Waziri ataandika kabisa barua ya kujiuzulu na inabakia kuweka tarehe tu ili akiboronga anawajibika bila hiyana. Uwajibikaji ni nguzo muhimu sana katika kuleta maendeleo nchini."

Lakini Zitto Kabwe aliweka sawa kuwa katika kipindi cha sasa ikitokea uchaguzi wa Oktoba hautofanyika au mwaka huu usipofanyika uchaguzi anaamini nchini itaingia katika machafuko. 

ACT Inatoa Wapi Pesa za Ziara
Moja wa shabiki wa ukura wa facebook alihoji kuwa pesa zinazosaidia cha cha ACT Wazalendo kuweza kufanya ziara zake mikoani tena kwa speed kubwa na ni chama kichanga hizo pesa wanatoa wapi ukizingatia kuna vyama vya siasa vipo miaka mingi sana lakini havijaweza kufanya hata ziara ndani ya mji wa Dar es Salaam sababu vinakosa pesa za kufanya hivyo, kiongozi huyo wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe alisema kuwa ni dhamira tu na yeye pesa za kufanya hivyo anachangiwa na wananchi wanaopenda harakati zake.

"Ni dhamira tu. Wapo watanziania wengi sana wanaoamini katika kazi za Zitto Kabwe hawawezi kukubali nishindwe kufanya siasa sababu ya fedha. Ninachangiwa hata na mama lishe."


Natamani Kujiunga UKAWA
Katika hatua nyingine Zitto Kabwe ameweka wazi kuwa katika moja ya mipango yao ilikuwa ni kuunganisha nguvu kama ambavyo awali ametuleza kuwa ili kujenga demokrasia imara ni lazima vyama vya siasa viweze kuunganisha nguvu zao hivyo anadai alitamani waweze kuungana na UKAWA katika kuona ni jinsi gani wanaweza kufumua mfumo wa uongozi ulipo sasa wa chama tawala ila akadai kuwa UKAWA walikataa.

Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe alimaliza kwa kuwaambia mashabiki kuwa kuna matapeli wanatumia jina lake na kujifanya wanatoa mikopo hivyo yeye hausiki nao na wananchi wanapaswa kutambua hao watu ni matapeli na amesema mara nyingi huwa anatoa taarifa sehemu husika juu ya watu wao.

"Hao ni matapeli. Akaunti yangu ni hii na Zitto Z Kabwe pekee. Nyingine ni watu tu wanatengeneza na huwa tunazitolea taarifa."-Zitto Kabwe

Lowassa na Dk. Slaa ni marafiki wa Gwajima? Wanachokitaka UKAWA kabla ya Uchaguzi 2014… Zisikilize kutoka #PB


Jumatatu ya April 06 kati ya stori zilizosikika kwenye uchambuzi wa MAGAZETI kwenye #PowerBreakfast iko ya Askofu Gwajima kusema hawezi kuwatupa Lowassa na Dk. Slaa kwa kuwa ni marafiki zake wa siku nyingi, UKAWA kuidai Serikali mambo manne kabla ya uchaguzi, na madereva kugoma kurudi shule kwa kuwa hawana mikataba ya ajira wanazofanya.

Stori nyingine inahusu mtoto mlemavu kufungiwa darini miezi minne, Polisi kujiua kwa kujipiga risasi katika kituo cha Polisi Tabora, iko nyingine ya waasisi wa CCM kukubali utafiti ulioonesha Prof. Mark Mwandosya anafaa kugombea Urais 2015.

Rais Kikwete amesema Serikali ya awamu yake inajivunia mafanikio, Waziri Bernard Membe amewataka vijana wasikubali kutumika, kuna stori pia ya watu 1665 kukosa makazi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Simiyu.

Imeandikwa pia kuhusu bunduki nyingine kupotea katika mazingira ya kutatanisha kituo cha Polisi Tabora, watoto 21 wazaliwa katika mkesha wa Pasaka Iringa, wapenzi waliokamatwa kwa kuuza tiketi za kwenda peponi Uingereza na waumini Shinyanga wakaguliwa kabla ya kuingia kwenye ibada ya mkesha wa Pasaka.
Hizi zilisikika kwenye show hiyo..
88.1 Clouds FM inasikika ukiwa Mwanza.
Kama ulipitwa bonyeza play hapa chini kusikiliza uchambuzi wa story zote za Magazeti ya leo…
 SIKILIZA HAPA

SAKATA LA JARIBIO LA KUUAWA, DR. SLAA ATINGA KITUO CHA POLISI




Dk. Slaa akihojiwa na wanahabari. ..Slaa (kulia), akitoka katika lango kuu la Kituo cha Polisi akiwa na viongozi wengine wa chama hicho.


Waandishi wa habari (kulia) wakimsubiri Slaa nje.Gari la Dk. Slaa likiwa limepaki nje ya Kituo cha Polisi Central.

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dr. Willbroad Slaa, ameripoti katika Kituo cha Polisi Central kilichopo Posta jijini Dar kuhusiana na sakata zima la mlinzi wake anayetuhumiwa kutaka kumuua.

Akizungumza na wanahabari kituoni hapo, Slaa alisema yeye hakuitwa na Jeshi la Polisi kujielezea bali kutokana na maneno yanavyozidi kusambaa na kuwasilishwa ndivyo sivyo ameona aende kueleza ukweli ulivyo.

Alisema kuwa, kwa mujibu wa chama chake, ameona ni vyema kwenda kulieleza Jeshi la Polisi kuhusiana na ishu nzima inayomkabili mlinzi wake, ambapo alikutana na Kamanda wa Kanda Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Suleimani Kova na kumueleza kila kitu kwa kuandika karatasi tisa (9) zenye maelezo yake, hivyo zoezi zima la kutoa taarifa kuhusiana na alichoandika ameliachia Jeshi la Polisi baada ya wao kufanya kazi yao ya Uchunguzi.

“Ndugu zangu wanahabari sijaitwa hapa kwa ajili ya mahojiano kama taarifa zinavyozaga lakini kutokana na uongozi nilionao nimeona ni vyema suala hili nilifikishe Polisi, na katika maelezo yangu nimeweza kuandika zaidi ya karatasi tisa (9) zenye ukweli mtupu, hivyo nimelikabidhi Jeshi la Polisi na baada ya wao kufanya uchunguzi litatoa taarifa kamili juu ya kile nilicho kiandika,’’ alisema Dr. Slaa.


(PICHA/STORI NA DENIS MTIMA/GPL)

HIVI KUNA HILA GANI KWENYE HILI LA KATIBA MPYA?

 

Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samweli Sita akisalimiana na rais Jakaya Mrisho Kikwete.


MWAKA huu unaingia katika historia ya nchi yetu moja kwa moja pasipo maswali. Tofauti na wakati mwingine, mwaka huu una uwezekano wa kupitisha matukio makubwa mawili, ambayo kwa namna yoyote, yanaweza kuharibu au kuimarisha taifa letu lenye umri wa miaka 50 tangu lipate uhuru wake.

Tukio moja tumelizoea kwa sababu tunalipitia kila baada ya miaka mitano, ambalo linahusu uchaguzi mkuu wa kutupatia rais, wabunge na madiwani mpya kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Hii itakuwa ni mara ya tano kwa wananchi kujipanga vituoni kufanya uchaguzi tangu tuanze mfumo wa vyama vingi, 1992.

Ingawa tangu tuanze kufanya hivyo mara zote Chama Cha Mapinduzi kimeibuka kidedea katika nafasi ya urais, kama inavyotarajiwa tena safari hii, lakini uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na changamoto nyingi, kwani kwa mara ya kwanza, CCM inahisi upinzani wana nafasi ya kushika dola, kutokana na kuimarika kwa kambi ya upinzani na migawanyiko ya ndani kwa ndani miongoni mwa makada wake.

Ni uchaguzi unaokuja huku wapinzani wakitangaza kuungana kwa kusimamisha mgombea mmoja kwa kila nafasi, kwa kila jimbo na kata, kupitia umoja wao wa Ukawa. Katika nchi ambayo imeamua kufuata misingi ya demokrasia, ya kuwaachia wananchi kumchagua kiongozi wanayemtaka, lolote linaweza kutegemewa katika kinyang’anyiro hiki kinachotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wake.

Lakini ukiachana na tukio hili, lipo lingine ambalo kinadharia linaonekana ni dogo lakini kiuhalisia ni kubwa na muhimu kuliko hata Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Hili linahusu kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa ambayo katika kalenda, inaonyesha kuwa wananchi watapaswa kupiga kura ya kuikubali au kuikataa Aprili 30, mwaka huu.

Wote tunajua kuwa upitishwaji wa Katiba hii katika Bunge Maalum la Katiba lililokuwa likiongozwa na Mhe. Samuel Sitta haukuwa mzuri, kwa namna ile tuliyoitarajia baada ya baadhi ya wajumbe kususia mchakato wake kwa madai ambayo tunayafahamu. Sitaki kurejea nyuma, juu ya uhalali wake, kwa sababu ninajua kwa mujibu wa sheria, Katiba Inayopendekezwa ni halali.

Tatizo langu limekuwa juu ya namna mamlaka zinazohusika zinavyolichukulia jambo hili kirahisi, kiasi kwamba wanaacha mambo ya msingi bila sababu zenye hoja. Kwa mfano, tunahitaji kujua idadi ya wananchi watakaokuwa na hadhi ya kuipigia kura katiba hii, ambao haina namna wanavyoweza kupatikana pasipo uandikishaji upya kufanywa na Tume ya Uchaguzi yaani NEC.

Hadi ninapoandika makala haya, bado hakuna hatua zilizo wazi juu ya nini kinafanyika kuhusu uandikishwaji huu. Lakini achana na hilo, kuna hili la kutoa elimu kwa wananchi juu ya nini kilichomo ndani ya katiba inayoelezwa kuwa ni yao, ili waijue, wajiandae kuikataa au kuikubali. Zoezi la kutoa elimu hii, haliwezi kufanywa kwa kutoa makala magazetini, linatakiwa kufanywa ‘live’ ili watu wawe na nafasi ya kuuliza na kujibiwa maswali.

Labda mamlaka zinapaswa kutambua kuwa suala hili siyo la kulifanyia majaribio wala masihara, kwa sababu halina hati miliki ya chama chochote cha siasa. Kama kuna watu wanadanganyana kuwa Watanzania wanaburuzika, ni sawa, lakini muhimu kwao kutambua kuwa wataburuzika leo, siyo kila siku.

Elimu ni lazima itolewe ili wananchi wapige kura itakayosukumwa na dhamira ya mioyo yao, tusiwafanye wapige kura kwa laghai, kwa sababu watakapogundua kuwa watawala waliwalaghai, inaweza kutuletea matatizo kuliko kama tungeweza kuzuia jambo hili leo, tena pasipo gharama yoyote.

Kama tunadhani tuna mambo mawili makubwa na muhimu, basi moja lisubiri. Hili la Katiba Inayopendekezwa lisubiri, tufanye uchaguzi, tuwapate viongozi wetu wapya, wakae na kuanza mchakato wa kura ya maoni, kwa sababu tutakuwa na muda wa kutosha, tofauti na hili la zimamoto linaloonekana kutayarishwa kufanywa na watawala wetu. Kinga ni bora kuliko tiba!
Older Posts
© Copyright VIJIMAMBOZI Published.. Blogger Templates
Back To Top