Kortini kwa Kumpa Mwanafunzi Mimba





MKAZI wa Mpiji Magoe Hamis Mohameid (21), amefikishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni Dar es Salaam akikabiliwa na tuhuma za kumbaka mwanafunzi (14)Jina limehifadhiwa na kumpa mimba. 

Akisomewa mashtaka mawili mbele ya Hakimu Flora Mtarania, Wakili wa Serikali Grace Lwila, alidai kuwa tukio hilo lilitokea kati ya Aprili na Mei24 mwaka huu maeneo ya huko Mpiji Magoe. 

Katika shtaka la kwanza Wakili alidai kwamba mtuhumiwa alimbaka msichana huyo kisha kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri. 

Wakili Lwila alidai kuwa katika shtaka la pili katika tarehe isiyojulikana maeneo ya Mpiji Magoe mtuhumiwa alimpa ujauzito mwanafunzi huyo wa kidato cha pili anayesoma shule ya Sekondari Mpiji Magoe. 

Mtuhumiwa alikana kutenda shtaka hilo na upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea ambapo Hakimu Mtarania alisema kwamba shauri hilo linadhaminika. 

“Unatakiwa ulete wadhamini wawili walioajiriwa kutoka serikalini au katika taasisi inayotambulika kisheria watakaoweka bondi ya maandishi ya Sh. Milioni 1,” alisema Mtarania. 

Hata hivyo mtuhumiwa alirudishwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti hayo na kesi hiyo itakuja tena Juni 24, mwaka huu.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright VIJIMAMBOZI Published.. Blogger Templates
Back To Top