MAMA wa mtoto aliyeibwa kabla hajatimiza mwezi tangu azaliwe, Fatuma Bakari ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala jinsi mtoto huyo alivyoibwa na mshtakiwa Neema Patrick.
Shahidi huyo na mwingine walitoa ushahidi wao jana mbele ya Hakimu Adelf Shachore kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Anunciata Leopold.
Awali mashahidi hao walikuwa watano ambao walifika mahakani kwa ajili ya kutoa ushahidi, lakini Wakili Leopold, alidai kuwa kwa mujibu wa shtaka hilo waliotakiwa kutoa ushahidi walikuwa wawili tu.
Wakitoa ushahidi wao mashahidi hao ambao ni Fatuma Bakari na Zainabu Said, wote walikiri juu ya mtuhumiwa kufanya kitendo hicho cha kuiba mtoto.
“Ni kweli siku ya tukio ambayo ni mwezi machi mwaka huu, mtuhumiwa alinisindikiza hospital nilipokuwa naumwa jino, kutokana na hali niliyokuwa nayo mtuhumiwa aliniomba anibebee mwanangu (Ibrahm Abdalah, ambaye hajatimiza hata mwezi) lakini mara baada ya kufika hospital maeneo ya Mbagala, Dar es Salaam, alishushuka haraka na kukimbia na mwanangu,” alidai Shahidi huyo.
Awali mashahidi hao walitakiwa kuwa watano lakini wakili wa serikali alipinga kutoa utetezi wao, hivyo mashahidi watatu walibaki ushahidi wao utasikilizwa Juni 24 mwaka huu.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumwiba mtoto huyo maeneo ya Mbagala Machi 3 mwaka huu ambapo alikuja kukamatwa baad ya wiki mbili maeneo ya Ukonga Banana akiwa na mtoto huyo, mtuhumiwa huyo yuko nje kwa dhamana.