Home » All posts
WANUSA KIFO,BODABOYA YAO YACHOMWA MOTO BAADA YA KUPORA MKOBA,SIMU
Vijana wawili wa bodaboda walikoswakoswa kuuawa baada ya kupora mkoba uliokuwa na simu wa mwanamke aliyekuwa akipita njia. Tukio hilo lilitokea Jumanne iliyopita, saa 1.30 usiku maeneo ya Sinza Afrika Sana, pembeni ya Baa ya Hongera ambapo inadaiwa ni eneo hatari kwa wizi huo.
Mmoja ya watuhumiwa akiwa hoi baada ya kupata kipigo
Shuhuda wa tukio hilo amesema kuwa tabia ya baadhi ya vijana kutumia usafiri wa bodaboda kupora watu simu na mikoba, hasa wanawake, imekua kawaida; na kwamba siku hiyo arobaini ya vijana hao ilikuwa imefika.
“Sisi tulikuwa pale baa tunakunywa, mara tukamsikia mtu akipiga kelele za mwizi…mwiziii, ile kutoka ndiyo tukawaona hawa vijana wawili wakihangaika kuwasha bodaboda yao ili wakimbie.
Askari polisi aliyeokoa maisha ya mtuhumiwa akiwa katika eneo la tukio
“Yaani ilikuwa ni Mungu tu maana bodaboda isingegoma kuwaka, tusingewapata. Basi raia wenye hasira kali wakaanza kuwashushia kipigo, aliyekuwa akiendesha pamoja na yule dada aliyeibiwa wakachukuliwa hadi Kituo cha Polisi Mabatini huku aliyekwapua akipewa kipigo,” alisema shuhuda huyo.
Hata hivyo, kijana huyo aliponea chupuchupu kuchomwa moto, kwani waliokuwa wamefuata mafuta ya petroli waliporudi walimkuta trafiki akizuia asiuawe.Kufuatia zuio hilo, raia hao walihamishia hasira zao kwenye kuichoma moto bodaboda kisha mtuhumiwa akachukuliwa hadi polisi kwa hatua zaidi za kisheria
Bodaboda iliyokuwa inatumiwa na vibaka hao ikiteketea kwa moto baada ya kuchomwa na washeria mkononi
Chanzo:globalpublishers.info
WEMA SEPETU ,AUNT EZEKIEL WATIBUANA KISA ZARI WA DIAMOND
Gazeti la Risasi la leo limeripoti kuwa Mataa wa bongo movies ambao ni mashosti wa kufa na kuzikana, Wema Isaac Sepetu na Aunt Ezekiel Grayson wanadaiwa kugombana baada ya Aunt ‘kuposti’ kwenye ukurasa wake wa Instagram tangazo lililohusiana na pati ya mwandani wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ iliyofanyika Mlimani City jijini Dar wikiendi iliyopita.
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa mastaa hao wa sinema za Kibongo, baada ya Aunt kuposti tangazo hilo akiwalaumu watu wa mtandao wa huduma za simu waliomtumia ndipo Wema akaona na kuja juu.
Ilielezwa kwamba baada ya Aunt kutupia picha ya tangazo hilo, Wema alichukizwa na kitendo hicho huku akimuona Aunt kuwa amemsaliti.
Ilisemekana kwamba katika utetezi wake, Aunt hakupendezwa na tangazo hilo alilotumiwa na mtandao huo wa simu.
“Wema alivyoona alichukia na kusema Aunt alikuwa akimsaliti na alitumia tangazo lile kijanja kwa ajili ya kuwatangazia watu kuhusu pati ya Zari wakati anajua kabisa kuwa Wema hazipandi na Zari kwa sababu anatoka na aliyekuwa mchumba’ke (Diamond),” kilisema chanzo hicho.
Katika sakata hilo, kuna watu ambao waliona Aunt hakuwa na kosa lakini wapo walioona hakuwa sahihi, jambo ambalo lilichochea ugomvi wao huku wakidaiwa kukesha wakitukanana.
Gazeti hilo lilipozungumza na Aunt kuhusiana na sakata hilo, alikiri kutokea akisema kuwa hakuwa na maana mbaya kuposti tangazo hilo lakini kila mtu ana mtazamo wake.
“Mimi sikumaanisha chochote kibaya kuhusu hilo tangazo na wala sikujua kama kuna mtu anaweza akalichukulia tofauti kabisa na hapo na mimi ndiyo nashindwa cha kuzungumza,” alisema Aunt.
Alipopigiwa Wema simu yake iliita bila kupokelewa.
ZITTO KABWE AFUNGUKA KUWA ALIPOFUKUZWA CHADEMA ALITAMANI KUJIUNGA NCCR-MAGEUZI.....SOMA HAPA
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amefunguka na kusema kuwa alipofukuzwa Uanachama katika chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alitamani kujiunga na Chama Cha NCCR-Mageuzi kwani ndicho chama ambacho kilikuwa kinaendana na itikadi yake anayoifuata na kuiamini ambayo ni itikadi ya Ujamaa.
Zitto Kabwe alifunguka haya jana alipokuwa akichat Live kupitia ukurasa wa facebook wa EATV katika kipengele cha KIKAANGONI .
Zitto Kabwe alisema kuwa alishindwa kujiunga na Chama hicho cha NCCR-Mageuzi kutokana na kuwepo kwa matatizo hivyo aliona siyo vyema kujiunga nacho, ndiyo maana alifikiri kuwa na chama cha siasa ambacho kitakuwa na misingi na itikadi ambayo yeye anaiamini na kuisimamia.
Katika hili moja ya shabiki alitaka kujua kwanini aliamua kujiunga na ACT Wazalendo na kuacha kujiunga na chama kilichokomaa kisiasa kama TLP,NCCR-Mageuzi,CUF, au CCM na majibu ya Zitto yalikuwa kama hivi.
"Nilifikiria hivyo pia lakini nikaona kuwa ni vema sasa kuwa na chama cha siasa ambacho kina itikadi ninayoifuata na kuiamini nayo ni itikadi ya Ujamaa.
"Chama cha NCCR-M mageuzi pekee ndio kinakaribia kuwa na itikadi hiyo lakini napo kulikuwa na matatizo ambayo kujiunga kwangu nao ingekuwa sio vema. Pili mimi ni mpiganaji.
Wengine wananiita jeshi la mtu mmoja! Sio kweli lakini. Hivyo kwenda chama kichanga ni ujasiri wa hali ya juu. Mungu atasaidia hakitakuwa chama kichanga baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2015".
"Mimi sio mwanzilishi wa ACT Wazalendo isipokuwa waanzilishi walikuwa watu ninaoshabihiana nao kwenye itikadi kama Prof. Kitila Mkumbo na Ndugu Mwigamba" Aliongeza Zitto Kabwe.
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo ambaye kwa sasa amekuwa akiitwa majina mengi ya ajabu ajabu kama msaliti,Yuda, kibaraka wa CCM na mengine mengi alisema kuwa hilo ni suala la kawaida katika siasa maaana hayo ni maneno tu ambayo hata baadhi ya viongozi wakubwa katika vyama vya siasa walishaitwa majina hayo ila anasisitiza jambo kubwa na la muhimu ni kumpima kwa kazi zake ambazo amezifanya bungeni katika kipindi chote alipokuwa mbunge na jinsi alivyoweza kujenga uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi.
"Hayo ni maneno ya kisiasa tu. Hata Marando aliwahi kuitwa Msaliti. CUF waliwahi kuitwa mashoga. NCCR na Mbatia waliwahi kuitwa pandikizi.
"Ni maneno ya kisiasa tu ambayo hayaongezi ugali kwenye sinia. Muhimu ni kuni judge kwa kazi ambazo nimefanya Bungeni katika kipindi changu. Kazi ya kujenga uwajibikaji."
Lakini mbali na kuonyesha kuwa kumekuwa na changamoto katika siasa za Tanzania hususani ndani ya vyama vya siasa Zitto Kabwe alizidi kusisitiza kuwa chama cha siasa ni itikadi hata hivyo umoja wa vyama vya siasa ni muhimu sana katika kujenga Demokrasia imara.
"Chama cha siasa ni itikadi. Hata hivyo umoja wa vyama ni muhimu sana katika kujenga demokrasia imara"
Uchaguzi Mkuu 2015
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo ameonyesha kuwa huenda kwa mwaka huu katika uchaguzi mkuu Tanzania ikaandika historia nyingine kwa Rais wa chama kimoja kukabidhi nchi kwa Rais wa chama kingine, hii inamaana kuwa huenda Rais Jakaya Kikwete akakabidhi nchi kwa Rais kutoka chama cha upinzani.
"Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Rais wa chama kimoja anaweza kukabidhi nchi kwa Rais kutoka chama kingine."
Lakini hapo hapo kiongozi huyo ndipo alipoonyesha wazi kuwa kwa upande wake yeye atagombea nafasi ya ubunge kupitia chama chake cha ACT Wazalendo na kusema kuwa mpaka sasa hajajua ni jimbo gani anakwenda kugombea nafasi hiyo ya ubunge.
"Nitagombea Ubunge mungu akipenda. Jimbo gani bado sijaamua"
Kutokana na hili mashabiki walihitaji kujua siku akiweza kufanikiwa kushika nafasi ya Rais wa nchi hii ni jambo gani la kwanza kuanza kufanya .
"Ikitokea nimekuwa Rais wa Tanzania Kila Waziri ataandika kabisa barua ya kujiuzulu na inabakia kuweka tarehe tu ili akiboronga anawajibika bila hiyana. Uwajibikaji ni nguzo muhimu sana katika kuleta maendeleo nchini."
Lakini Zitto Kabwe aliweka sawa kuwa katika kipindi cha sasa ikitokea uchaguzi wa Oktoba hautofanyika au mwaka huu usipofanyika uchaguzi anaamini nchini itaingia katika machafuko.
ACT Inatoa Wapi Pesa za Ziara
Moja wa shabiki wa ukura wa facebook alihoji kuwa pesa zinazosaidia cha cha ACT Wazalendo kuweza kufanya ziara zake mikoani tena kwa speed kubwa na ni chama kichanga hizo pesa wanatoa wapi ukizingatia kuna vyama vya siasa vipo miaka mingi sana lakini havijaweza kufanya hata ziara ndani ya mji wa Dar es Salaam sababu vinakosa pesa za kufanya hivyo, kiongozi huyo wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe alisema kuwa ni dhamira tu na yeye pesa za kufanya hivyo anachangiwa na wananchi wanaopenda harakati zake.
"Ni dhamira tu. Wapo watanziania wengi sana wanaoamini katika kazi za Zitto Kabwe hawawezi kukubali nishindwe kufanya siasa sababu ya fedha. Ninachangiwa hata na mama lishe."
Natamani Kujiunga UKAWA
Katika hatua nyingine Zitto Kabwe ameweka wazi kuwa katika moja ya mipango yao ilikuwa ni kuunganisha nguvu kama ambavyo awali ametuleza kuwa ili kujenga demokrasia imara ni lazima vyama vya siasa viweze kuunganisha nguvu zao hivyo anadai alitamani waweze kuungana na UKAWA katika kuona ni jinsi gani wanaweza kufumua mfumo wa uongozi ulipo sasa wa chama tawala ila akadai kuwa UKAWA walikataa.
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe alimaliza kwa kuwaambia mashabiki kuwa kuna matapeli wanatumia jina lake na kujifanya wanatoa mikopo hivyo yeye hausiki nao na wananchi wanapaswa kutambua hao watu ni matapeli na amesema mara nyingi huwa anatoa taarifa sehemu husika juu ya watu wao.
"Hao ni matapeli. Akaunti yangu ni hii na Zitto Z Kabwe pekee. Nyingine ni watu tu wanatengeneza na huwa tunazitolea taarifa."-Zitto Kabwe
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WZ ELIMU YA JUU YAANZA KUPOKEA MAOMBI YA MIKOPO KUTOKA WA WANAFUNZI KWA MWAKA WA MASOMO 2015/2016
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jana (Ijumaa, Mei 1, 2015) imetoa mwongozo kwa wanafunzi wahitaji wanaotarajia kuomba mikopo na ruzuku kwa ajili ya mwaka wa masomo 2015/2016 unaotarajiwa kuanza miezi michache ijayo.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, ambao unapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz), waombaji wote wamepewa takribani miezi miwili kuwasilisha maombi yao kuanzia Jumatatu, Mei 4, 2015 hadi Jumanne, Juni 30, 2015.
Aidha, wanafunzi wote wahitaji wa mkopo na ruzuku wanapaswa kufanya na kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia mfumo maalum (Online Loans Application and Management System) ulioanzishwa na HESLB kwa ajili ya kupokea maombi hayo. Mfumo huo unapatikana kupitia tovuvi ya Bodi au kwa kufungua kiunganishi chake (http://olas.heslb.go.tz).
Pamoja na mambo mengine, mwongozo huo unafafanua kuwa waombaji wa mara ya kwanza (First Time Applicants) wanapaswa kulipa ada ya maombi ya Tshs 30,000/- kwa na kisha kutumia namba ya muamala (Transaction ID) kuingia katika mtandao na kuanza kujaza fomu za maombi.
“Waombaji wa mara ya kwanza wanapaswa kulipa ada ya maombi ya Tzs 30,000/- ambayo inalipwa mara moja tu na haitarudishwa kwa nia ya M-Pesa,” inasema sehemu ya mwongozo huo uloiotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo.
Aidha, mwongozo huo umesisitiza kuwa wanafunzi wenye mikopo na wanaoendelea na masomo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu hawapaswi kuwasilisha maombi tena.
Bodi imewasihi waombaji na wadau wengine kuusoma na kuuzingatia muongozo huo wakati waote wanapofanya na kuwasilisha maombi.
HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu.
Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.
-SOURCE:MPEKUZI














































